Maneno Husika ya Mungu:
Wale ambao wanaweza kufuata kazi ya sasa ya Roho Mtakatifu, na ambao wanaweza kuzifuata nyayo za Mungu, kiasi kwamba wamfuate Mungu popote Awaongozapo—hawa ni watu ambao wamebarikiwa na Mungu. Wale wasiofuata kazi ya sasa ya Roho Mtakatifu hawajaingia katika kazi ya maneno ya Mungu, na haijalishi wanafanya kazi kiasi gani, au mateso yao ni makubwa vipi, au wanakimbia hapa na pale kiasi gani, hakuna linalomaanisha chochote kwa Mungu kati ya hayo, na Yeye hatawasifu. Leo, wale wote ambao hufuata maneno halisi ya Mungu wako ndani ya mkondo wa Roho Mtakatifu; wale ambao ni wageni kwa maneno halisi ya Mungu wako nje ya mkondo wa Roho Mtakatifu, na watu hao hawasifiwi na Mungu. Huduma ambayo imetenganishwa na matamshi halisi ya Roho Mtakatifu ni huduma ambayo ni ya mwili, na ya dhana, na haiwezi kuwa kwa mujibu wa mapenzi ya Mungu. Kama watu huishi miongoni mwa dhana za kidini, basi hawawezi kufanya lolote lenye kustahili kwa mapenzi ya Mungu, na hata ingawa wao humhudumia Mungu, wao huhudumu katikati ya mawazo na dhana zao, na hawawezi kabisa kuhudumu kwa mujibu wa mapenzi ya Mungu. Wale ambao hawawezi kuifuata kazi ya Roho Mtakatifu hawaelewi mapenzi ya Mungu, na wale ambao hawaelewi mapenzi ya Mungu hawawezi kumhudumia Mungu. Mungu hutaka huduma inayoupendeza moyo Wake mwenyewe; Hataki huduma ambayo ni ya dhana na mwili. Kama watu hawawezi kuzifuata hatua za kazi ya Roho Mtakatifu, basi wao huishi katikati ya dhana, na huduma ya watu hao hukatiza na huvuruga. Huduma hiyo huenda kinyume na Mungu, na hivyo wale ambao hawawezi kuzifuata nyayo za Mungu hawawezi kumhudumia Mungu; wale ambao hawawezi kuzifuata nyayo za Mungu humpinga Mungu bila shaka, na ni wasioweza kulingana na Mungu.